Ujamaa na Zanzibar
Published on May 7, 2025
Tulifanya safari kuelekea Zanzibar, haswa kisiwa cha Unguja, mnamo Aprili 2025. Safari hii ilikuwa ya utalii, tulitaka kuchunguza uzuri wa maeneo ya Zanzibar. Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kufika Zanzibar, hivyo ilikuwa fursa ya kipekee. Safari ilikuwa ndefu, na tulipitia maeneo mbalimbali ya Kenya na bara la Tanzania, lakini katika blogu hii nitajikita kuzungumzia Zanzibar pekee.

Stone Town
Tanzania na Falsafa ya Ujamaa
Tanzania (Tanganyika na Zanzibar) kwa ujumla inajulikana kwa kuwa na ujamaa. Ujamaa ni neno la Kiswahili linalomaanisha familia au jamii, na linaakisi dhana kwamba mtu hutambulika na kustawi kupitia ushirikiano na mshikamano wa watu wengine. Ujamaa ni ile hali ya kuishi na udugu na kila mtu.
Mwalimu Julius Nyerere alichukua dhana ya Ujamaa na kuifanya kuwa msingi wa maendeleo ya taifa la Tanzania. Kwa mujibu wake, Ujamaa haukuwa tu falsafa ya kijamii bali pia mfumo wa kisiasa na kiuchumi uliolenga kuleta usawa na kujitegemea. Alifafanua Ujamaa kupitia nguzo kadhaa:
- Mfumo wa chama kimoja
- Usawa wa kijamii, kiuchumi na kisiasa
- Uzalishaji vijijini
- Kujitegemea
- Elimu kwa wote
Zanzibar: Kisiwa chenye Historia Tajiri
Zanzibar ni kisiwa chenye mandhari ya kupendeza na utulivu wa kipekee. Ufukwe wake una mchanga mweupe na maji ya rangi ya samawati ang'avu, vinavyovutia wageni kutoka pande zote za dunia. Mji Mkongwe (Stone Town), ambao ni urithi wa dunia wa UNESCO, ni kielelezo cha mchanganyiko wa tamaduni za Kiarabu, Kiafrika, Kihindi, na Ulaya. Mitaa yake midogo yenye majengo ya kale ya mawe, milango ya nakshi, na harufu ya viungo huifanya Zanzibar kuwa mahali pa kipekee kihistoria na kiasili.

Ufukwe
Kabla ya Mapinduzi ya 1964, Zanzibar ilikuwa chini ya utawala wa Kisultani. Jamii ilikuwa imegawanyika kitabaka—wachache wa Kiarabu walikuwa na mali na mamlaka, huku Waafrika wengi wakiwa katika hali ya unyonge. Hali hii ilisababisha msuguano wa kijamii na kisiasa, uliopelekea Mapinduzi ya Januari 12, 1964. Serikali mpya ilianzisha mageuzi ya kijamaa kama kugawa ardhi kwa wakulima, kufuta mashamba ya kifahari, na kusambaza huduma za afya na elimu bila malipo. Lengo lilikuwa kuondoa matabaka na kuleta usawa wa kijamii, msingi muhimu wa sera za Ujamaa.
Mnamo Aprili 26, 1964, Zanzibar na Tanganyika ziliungana na kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Muungano huu haukuwa wa kisiasa tu, bali pia wa kijamii na kiuchumi. Uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere (Tanganyika) na Abeid Karume (Zanzibar) uliimarisha misingi ya Ujamaa na Kujitegemea kupitia Azimio la Arusha la mwaka 1967. Zanzibar, ikiwa na historia ya mapinduzi, ilitoa mchango wa dhati katika kuendeleza wazo la taifa linalojali usawa na maendeleo kwa wote. Ingawa changamoto za kiutendaji zilibaki, mwelekeo wa pamoja wa siasa za kijamaa uliendelea kuongoza taifa.
Ujamaa kwa Vitendo: Nilichojifunza Kutoka kwa Watu
Kama wewe umekulia bara, utapigwa na mshangao mkubwa utakapoenda Zanzibar. Ningesema, Zanzibar bado imehifadhi maadili ya Ujamaa kwa kiwango cha juu. Miji kama Dar es Salaam na Arusha imeathirika kwa kiasi kikubwa na "westernization" (magharibi-shaji). Tanga nayo inajitahidi kuhifadhi maadili hayo. Watu wa Tanga hata watakuonya kuwa ukienda Dar es Salaam, uwe mwangalifu kwani unaweza kulaghaiwa.
Katika safari yetu, tulianzia Tanga, tukapitia Dar es Salaam, kisha Zanzibar, kabla ya kurudi kupitia Moshi. Tulipokuwa Tanga, tulihudumiwa na mhudumu mmoja mkarimu katika mkahawa mmoja. Nakumbuka akimwambia rafiki yangu, "Si lazima uagize mishikaki leo, tunaweza kula kuku wa kuchoma halafu ukihisi njaa baadaye tutaagiza mishikaki." Tulipigwa na butwaa! Hii ni tofauti sana na hali ya bara, hasa Nairobi, ambapo biashara mara nyingi huendeshwa kwa tamaa ya faida pekee bila kujali mteja. Mhudumu huyu alitushauri hata sehemu ya kutembelea tulipofika Dar es Salaam. Hata wale waliokuwa hawatoi kidokezo walikiri kwamba huduma aliyotoa ilikuwa bora kiasi cha kutoa kidokezo kwa hiari.
Tulipoingia Zanzibar, tulikutana na dereva wa magari ya utalii aitwaye Adam. Tulipokuwa tukikubaliana bei, alisema, "Mimi sitafuti pesa, nataka mridhike ili mkienda bara muwashauri wengine waje Zanzibar." Huku Nairobi, hali ingekuwa tofauti kabisa. Badala ya kutupeleka moja kwa moja hotelini kama ilivyopangwa, alituelewa na kutupeleka kutalii sehemu tulizotamani—Mji Mkongwe, Forodhani, makumbusho ya Freddie Mercury, na spice farm—bila kuongeza gharama.
Tulipogundua kuwa hoteli yetu haikuwa Kaskazini (Nungwi) bali Mashariki, tulivurugika kidogo. Hatukutaka kurudi nyuma kwani shughuli nyingi tulizopanga zilikuwa Kaskazini. Adam alitupatia suluhisho—akatuunganisha na rafiki yake aliyekuwa na hoteli nafuu kule Kaskazini, ambako tulilala kwa siku mbili zilizofuata. Ingawa yeye alikuwa tu dereva, alitushughulikia kama rafiki wa dhati.

Tulipokuwa tukirudi, tulipitia Moshi. Katika harakati zetu, nilipanda pikipiki kwa Tsh 1,000. Dereva wa pikipiki alinihadaa —nilipompa elfu tano ili atafute chenji, alitoweka na pesa zangu. Hapo ndipo niligundua kuwa huku bara, "kila mtu kivyake, Mungu kwa wote."
Hitimisho
Safari yetu ya kuelekea Zanzibar haikuwa tu ya kutalii, bali pia ilikuwa safari ya kujifunza kuhusu historia, watu, na maadili ya kijamii yaliyokita mizizi ndani ya jamii ya Wazanzibari. Nilichojifunza zaidi ya yote ni kuwa Ujamaa bado unaishi—si kama sera ya kisiasa, bali kama mtindo wa maisha unaoonyeshwa kupitia ukarimu, mshikamano, na kujali wengine bila kutarajia malipo.
Moja ya matukio yaliyoacha alama ni pale tulipokuwa tukizungumzia kuhusu maeneo ya jirani na Zanzibar. Adam, dereva wetu wa utalii, alitueleza kuhusu kisiwa kingine kilicho karibu na Zanzibar ambako, kwa maneno yake, “watu bado wanaishi kama babu zao walivyoishi. Huko kuna ujamaa hata kuliko Zanzibar yenyewe. Hata barabara zimeanza kujengwa hivi karibuni tu.” Kauli hii ilinisisimua—ikawa mfano hai wa namna jamii hizi zimehifadhi thamani ya pamoja, kinyume na hali ya kibiashara inayotawala maeneo mengi ya bara.

Kutokana na uzoefu huu, najikuta nikitafakari: Je, Ujamaa ni dhana inayoweza kufufuliwa au kurekebishwa kwa kizazi cha sasa? Jibu langu ni ndiyo—lakini si kwa njia ya sera kali au kaulimbiu tupu, bali kupitia vitendo vidogo vya kila siku: kuwajali wenzetu, kusaidiana, na kutanguliza utu kabla ya faida.
Katika jamii ya sasa yenye mashindano makali na ubinafsi uliopitiliza, kuna haja ya dhati ya kutafakari upya kuhusu thamani ya mshikamano wa kijamii. Dunia ya leo imejaa mbio, presha, na mawasiliano ya kidijitali lakini yenye upweke mkubwa. Ujamaa unaweza kuwa daraja la kurejesha utu, maana ya kuwa sehemu ya jamii, na faraja ya kuwa si peke yako katika maisha haya.
Mwito wangu ni huu: Hebu kila mmoja wetu afikirie, ni mara ngapi tumewasaidia wenzetu bila kutarajia kitu? Ni mara ngapi tumetanguliza ustawi wa jamii kuliko manufaa binafsi? Labda, kupitia hatua ndogo kama hizo, tunaweza kuufufua Ujamaa—sio kama kumbukumbu ya kihistoria, bali kama njia ya kisasa ya kuishi kwa ubinadamu.
Subscribe to get future posts via email